Saturday, November 12, 2016

PACHA WANAO FANANA :1

RIWAYA:Pacha Wanaofanana

MTUNZI:Agness Matimba

SIMU:0757 143665/0714 215231

SEHEMU YA KWANZA.

ILIKUWA ni majira ya saa tatu za usiku. Mvua ya rasharasha ilikuwa imetanda katika kijiji cha Mtakuja,huku katika nyumba moja iliyokuwa kuu kuu ambayo haijulikani kwa mara ya mwisho ilifanyiwa ukarabati lini.Iilisikika sauti ya Bibi mmoja aliyejulikana kwa jina la Bi.Nyamtaka.Ilikuwa ikisisitiza kwa sauti,
"Catherine jitahidi sukuma,sukuma kwa nguvu.Mbona huyu mmoja ameshatoka".Sauti ya Catherine ikasikika,
"Siwezi Bibi nimechoka jamani",
"Jikaze mjukuu wangu, upo tayari kumpoteza mwanao?".Bi.Nyamtaka aliuliza,lakini ghafla chupa ya uzazi ilimalizika kupasuka.
Bi.Nyamtaka alimlaki mtoto kwa mikono miwili huku akimpokea kwa kusema.
"Ni wa kike tena. Wote ni wa kike".Catherine akatamka kwa sauti yenye uchovu,
"Kulwa ataitwa Maria na Doto ataitwa Mariam".
Bi.Nyamtaka alimfunga Kulwa kwa kutumia khanga ya bluu halafu Doto alimfunga khanga ya bluu bahari.Catherine alifurahi sana baada ya watoto kupatiwa huduma muhimu.
Catherine alipatiwa wanae aliwanyonyesha huku akiwaangalia kwa kutumia mwanga hafifu wa koroboi kuu kuu ambayo nayo kama ile nyumba, haijulikani kwa mara ya mwisho ilifanyiwa usafi lini.Baada ya kuwanyonyesha watoto wake hatimaye Catherine alilala usingizi mzito huku watoto wakiangaliwa na Bi.Nyamtaka.
***********
Siku iliyofuatia Bi.Nyamtaka akawa anawaangalia watoto wanatofauti gani katika miili yao maana walifanana sana.Na alimwambia Catherine kuwa kama watoto wale hawatagundulika na tofauti ni lazima moja atamtoboa katika sehemu ya mwili wake.
Hakika walikuwa ni watoto wazuri. Walifanana kila kitu.Kwa bahati nzuri Bi. Nyamtaka akagundua tofauti moja Kulwa alikuwa na alama ya kidoti kidogo sana karibu na pua, lakini Doto hakuwa nayo hivyo alimueleza Catherine na kumuonyesha asije akawachanganya.
***********
Catherine aliwapenda sana watoto wake, huku Bi.Nyamtaka akijitahidi kumsaidia kwa ukaribu kabisa kuwalea watoto wake kwa kuwapa malezi bora.
Catherine alikuwa mtu wa kukaa nyumbani.Bi.Nyamtaka akawa anapika pombe za kienyeji kwaajili ya kuwapatia kipato ambacho Kitamsaidia yeye na Catherine kwa kupata chakula na mavazi.Hata hivyo Catherine alijisikia vibaya sana akaona anampa mzigo Bibi yake.Hivyo moyoni alipanga yake,hakutaka kukaa sana kwa Bibi yake.
Baada ya miezi mitatu watoto wake walikuwa wamekuwa wakubwa kidogo wakiwa na afya tele.Catherine alianza kuwanywesha uji maana walishaanza kumchosha kwa sababu walikuwa wananyonya sana.
Siku moja jioni Catherine akiwa amekaa na Bibi yake nyumbani ndipo alipoamua kutoa dukuduku lake la moyoni kwa kumwambia Bibi yake anamaongezi naye muhimu.Bi.Nyamtaka bila ya hiyana akamwambia Catherine,
"Nakusikiliza mjukuu wangu niambie"Catherine alisawazisha koo lake vizuri kwa kukohoa kidogo.Huku akimwangalia Bibi yake,akaanza
"Ahsante sana Bibi kwa kunipokea na kunitunza tangu nilipokuja hapa kijijini nikiwa na mimba ya miezi miwili.Sasa hivi najiona kama nimekuletea mzigo mkubwa wa vitukuu wawili na mimi nahitaji kula pamoja na mavazi".Akatulia kidogo na kumuangalia Bibi yake aone atasemaje. Alipoona kimya,akaendelea,
"Nimeona nakuletea mzigo mkubwa sana hivyo nakuomba niruhusu niende mjini nikatafute maisha kwaajili ya wanangu, ikiwezekana na wewe pia niwe nakutumia hela kidogo kwaajili ya matumizi".Bi Nyamtaka alishtuka,akasimama huku akijifunga vizuri kanga yake kuu kuu iliyokuwa imetoboka.Akamwambia Catherine,
"Mjukuu wangu sikuruhusu kuondoka. Unatakiwa ukae nyumbani uwalee watoto wako.Isitoshe una watoto mapacha utaweza kuhimili mikikimikiki ya safari pamoja na kuwabeba watoto?"
"Ndio nitaweza Bibi naenda kutafuta maisha Bibi kwaajili ya wanangu na wewe Bibi. Wewe ndiye mlezi wangu uliyebaki kwaajili yangu, Bibi tafadhali niruhusu"Catherine alikuwa amemjibu Bibi yake hivyo.
Bi. Nyamtaka alikataa katukatu, hakumruhusu Catherine kurudi mjini tena.Catherine alikosa raha, alikaa kwa Bibi yake kwa shingo upande akiwaza afanye nini ili Bibi yake amkubalie kuondoka.
Baada ya siku tatu Catherine akiwa amejipumzisha alipata wazo akubaliana na wazo lake akapanga cha kufanya,wazo lililokuwa kichwani mwake ni kutoroka pale kwa bibi yake.
[SAFARI YA KUTOROKA]
Alfajiri Catherine alishtuka kutoka usingizini, akaamka na kumwamsha Bi.Nyamtaka kwaajili ya kujiandaa kuelekea sokoni.Bi.Nyamtaka akamshukuru Catherine kwa kumwamsha.
Bi.Nyamtaka alipoondoka.Catherine alianza kukusanya nguo za wanae na za kwake akaziweka kwenye rambo vizuri,na kwa bahati nzuri kulikuwa na begi lililokuwa limetoboka kwa kushambuliwa na panya pamoja na mende,hivyo mfuko ule wa rambo akauweka ndani ya begi lile.
Hakutaka kuoga. Alichukua maji akasukutua, akawabeba watoto wake. Mmoja alimbeba mgongoni mwingine akambeba mkononi. Kabla ya kuondoka akaangalia chini ya kitanda, kulikuwa na chungu kidogo ambacho Bi.Nyamtaka alipenda kuhifadhia hela za akiba.
Alikuta akiba wa shilingi elfu ishirini akaichukua na kuandika ujumbe kwa herufi kubwa.
BIBI USINITAFUTE NARUDI KWETU, NIMEYACHOKA MAISHA YA HAPA KIJIJINI.Catherine akaondoka.
Alitembea kwa miguu huku akiwa amevaa khanga zilizotoboka na kandambili tofauti ambazo zinajulikana kwa jina la almaarufu kama la "papa na nguru".Baada ya kutembea kwa muda wa nusu saa huku anga likiwa limetanda na ukungu mweupe wa asubuhi,ndipo alifanikiwa kufika kituo cha mabasi yaendayo mikoani.
Catherine alifanikiwa kupata basi ambalo lilikuwa likitokea pale kijijini kwao na kuelekea jijini Dar-es-salaam.Catherine akaingia kwenye basi na kupishwa siti na kijana wa makamo. Kisha mtoto wake mmoja akasaidiwa na mama mmoja aliyekuwa amekaa siti ya jirani yake. Hapo ndipo akapata afueni kidogo.Akiwa amempakata Maria, Catherine akawa anawaza huku analia.Alijikuta akisema kwa sauti kubwa
"Sitamsamehe".Yule mama aliyemsaidia mtoto akamuuliza,
"Hutamsamehe nani?"Catherine alibaki kimya, akaishika khanga yake iliyokuwa imetoboka akajifuta machozi huku akisema...

JE CATHERINE ALISEMA NINI?

ITAENDELEA KESHOKTWA JUMAMOSI******.

No comments:

Post a Comment

Iblame my body

RIWAYA   : I'BLAME MY BODY ( NAULAUMU MWILI WANGU ) Imezaminiwa na   Simulizimahiri.blogspot.com Mahakama kubwa ya kesi za jina...